Shaykh Swaalih Aalush-Shaykh kuhusu tofauti iliyopo ya kufupisha swalah        

Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

06- Abu ´Abdillaah an-Nu’maan bin Bashiyr (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa alimsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“…. yule anayeepuka vyenye shaka atakuwa amejisafisha kwenye dini yake na heshima yake.”

Haya ndio waliyofahamu wanachuoni kutokana na Hadiyth hii: juu ya kwamba kutoka katika tofauti za wanachuoni imependekezwa. Bi maana mtu kutoka kwenye tofauti zao na kwenda katika lile lililo na yakini ni jambo limependekezwa. Hili ni sahihi kwa njia fulani. Mfano wa hilo ni suala la kuhusu kufupisha swalah katika safari. Jamhuri ya wanachuoni wane – Maalik, Abu Haniyfah, Shaafi´iy na Ahmad – wameweka mpaka wa muda kwa yule aliyeweka nia ya kubaki [kwenye mji] siku nne na si zaidi ya hapo. Bi maana akinuia kubaki zaidi ya hapo hana ukhusa ya kufupisha swalah.

Kuna kauli nyingine ya Hanafiyyah inayosema kuwa ana ukhusa ya kufupisha swalah midhali hakupanga kubaki zaidi ya siku kumi na tano.

Vilevile kuna kauli nyingine ya tatu ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na wanachuoni wengine inayosema kuwa ana ukhusa ya kufupisha swalah mpaka pale ataporejea katika mji wake.

Kauli ya kwanza – ambayo amenuia kukaa siku nne – imepewa nguvu juu ya zingine kwa njia ya kwamba masuala haya ni yenye kutatiza kwa kuziangalia dalili. Mambo yakishakuwa ni hivyo, kutendea kazi yakini ni kujisafisha na dini kwa kuwa swalah ni nguzo ya Uislamu ya pili. Kutendea kazi yakini katika jambo hili la swalah ni miongoni mwa mambo yanayotolewa dalili na Hadiyth hii kwa kuwa ni kujisafisha na dini. Kwa sababu kufupisha swalah kwa aliyenuia kukaa chini ya siku nne ni jambo lenye makubaliano [kwa wanachuoni wote]. Ama maoni mengine wametofautiana kwayo. Mambo yakishakuwa ni hivyo, kutoka katika tofauti ni jambo limependekezwa. Hivyo tunachukua kauli yenye usalama. Wanachuoni wengi wahakiki wameipa nguvu kauli hii kwa njia ya kujisafisha na kwamba kuichukua kuna yakini juu ya jambo la swalah ambayo ni nguzo ya pili katika Uislamu na ndio nguzo kubwa ya kimatendo.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Arba´iyn an-Nawawiyyah, uk. 151-153
  • Imechapishwa: 17/05/2020